Monday, July 12, 2010

DNA test....!!!!

Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, imesema nusu ya watu waliokwenda kupima vinasaba (DNA) kutokana na kuwa na mashaka haya na yale, vipimo vimeonyesha kuwa si wazazi halisi wa watoto waliopimwa.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Vifaa na Matengenezo wa ofisi hiyo, Emmanuel Gwae, wakati akizungumza katika maonyesho ya biashara yanayofanyika katika viwanja vya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere.

Alisema tangu huduma hiyo ianze kutolewa na taasisi hiyo mwaka 2005, watu zaidi ya 2,000 walifika kupata vipimo kujua uhalisia wa watoto wao.

Alisema karibu nusu ya watu hao waliofika na kupimwa ilibainika kuwa watoto waliokuwa nao hawakuwa wa kwao.

Alisema idadi ya watu wanaokwenda kupata vipimo imekuwa ikiongezeka kuliko miaka iliyopita.

“Huduma hii ni kama imechelewa maana watu wanakuja kwa wingi sana kupima uhalisia wa watoto wao na wengi wanaopimwa wanakuta watoto si wao,” alisema.

Alisema kuna sababu nyingi zinazoweza kusababisha matokeo hayo ikiwemo kubadilishana watoto wakati wa kujifungua.

Alisema katika hospitali zenye mlundikano mkubwa wa wanawake wanaojifungua, baadhi ya wanawake kwa makusudi wanaweza kuwabadilishia wenzao watoto.

Alisema hali hiyo pia inaweza kutokea hata bila kukusudia kutokana na mazingira ya hospitali.

Alisema vipimo vya DNA hugharimu shilingi 300,000 na mhusika anaweza kupata majibu ndani ya wiki moja.

Alisema kabla ya mhusika kwenda kupata vipimo lazima apeleke kwa mkemia barua kutoka mahakamani, kwa wakili au ofisi ya ustawi wa jamii na kueleza sababu ya kutaka kupima.

__._,_.___

No comments:

Post a Comment